PAMBANO la mkondo mmoja wa kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya timu yake dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, linatarajiwa kuwa kipimo tosha cha uwezo wa kocha mpya wa Simba, Mosses Basena kutoka Uganda.
Basena, aliyetua Simba kumrithi Mzambia, Patrick Phiri, anatarajiwa kuiongoza Simba katika mechi hiyo itakayochezwa wiki ijayo kwenye uwanja huru, ambapo wadau wa klabu hiyo watataka kuona kama ataivusha kwenda hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ya Afrika.
Kocha huyo aliyekuwa akiinoa timu ya taifa ya Uganda kama kocha msaidizi, hilo litakuwa ni pambano lake la kwanza kuiongoza Simba kwenye michuano yoyote tangu aliposaini mkataba wa miaka miwili wa kuinoa timu hiyo mapema mwezi huu.
Simba ilipata fursa ya kuumana na Waydad baada ya kushinda rufaa yake iliyokata Shirikisho la Soka Afrika, CAF, dhidi ya waliokuwa mabingwa watetezi wa Afrika, TP Mazembe ya DR Congo iliyokuwa imezitung'oa timu zote hizo mbili kwenye michuano hiyo ya Afrika.
Kupata fursa hiyo ya kucheza pambano hilo, Simba inayoendelea kujifua chini ya Basena, aliyekatisha mapumziko yake na kuanzisha programu maalum kwa ajili ya kuiweka vema timu hiyo, inapaswa kushinda ili kudhihirisha kuwa 'ngekewa' iliyoipata ilikuwa ni haki yao kwelikweli.
Licha ya kwamba hata kama timu yao itafungwa na wapinzani wao, bado itaendelea kucheza mechi za kimataifa kwa kushiriki Kombe la Shirikisho, wadu wengi wa Msimbazi wangependa kuona Simba ikifuzu hatua hiyo ili kuwaziba midomo watani zao wanaowakejeli mitaani.
Yanga, ambao awali waliibeza Simba kwa kusumbuka kukata rufaa hiyo, hivi sasa wameibuka upya wakikejeli nafasi iliopata watani zao kwa kudai itaishia 'kunawa' mbele ya Waydad, hivyo wana Msimbazi wangependa kuona kocha wao mpya akiwapa raha.
Basena, anayeendelea kuwafua wachezaji kwa mazoezi kabambe, tayari ameanza kuonyesha sio kocha wa mchezo na huenda akaisaidia Simba sio kwenye michuano hiyo ya kimataifa, bali hata kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo msimu huu walipoteza taji kwa watani zao, Yanga.
Hii inatokana na jinsi anavyowanoa wachezaji wake kwenye uwanja wa Taifa, akiwaweka tayari kukabiliana na Waarabu hao ambao hawana rekodi ya kutisha barani Afrika kama timu zingine za ukanda huo wa Afrika Kaskazini.
No comments:
Post a Comment