VIMWANA waliojitokeza kushiriki shindano la Kimwana wa Twanga Pepeta 2011, wameanza kupata mafunzo ya ujasiriamali yanayolenga kuwapa ujuzi wa kuendesha biashara mbalimbali.
Kwa mujibu wa mratibu wa shindano hilo, Maimatha Jesse, vimwana 23 wamejitokeza kuwania taji hilo, ambapo kwa sasa wanaendelea kujifua chini ya mkufunzi wao 'Super K' na Matron Husna Idd 'Sajent'.
"Shindano la mwaka huu mshindi atazawadiwa duka la vipodozi, ndio maana tumewaletea wataalam wa mambo ya biashara ambao huwapa mafunzo ya ujasiriamali vimwana wetu," alisema Maimatha.
Maimatha alisema, kutokana na zawadi hiyo, vimwana hao wamekuwa wakifanya mazoezi, kisha kupewa elimu hiyo ambayo anaamini itawasaidia sio tu kwenye shindano hilo bali pia katika shughuli zao binafsi.
Alifafanua, zawadi za washindi wa tatu na wa nne zitatangazwa mara baada ya kufanyika shindano la nusu fainali ambalo litabakiza vimwana 10 tu kati ya hao 23 wanaoendelea na mazoezi sasa.
Maimatha alisema, shindano la nusu fainali litafanyika Mei 27 ndani ya ukumbi wa Club Sun Cirro, Sinza Dar es Salaam na vimwana 10 watakaobaki ndio watachuana kwenye fainali.
Fainali za michuano hiyo zitafanyika Juni 3, kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee kama mipango yao itaenda vema.
No comments:
Post a Comment