Monday, May 30, 2011

Chumo kuzinduliwa bure j'mosi

FILAMU mpya ya kimataifa ya 'Chumo' inatarajiwa kuzinduliwa bure kwenye viwanja vya Biafra, Kinondoni Dar es Salaam, siku ya Jumamosi uzinduzi utakaosindikizwa na makundi ya muziki ya Ashimba na Jagwa Music.
Uzinduzi wa filamu hiyo inayohusiana na masuala ya mapenzi, lakini yenye kuelimisha juu ya ugonjwa wa Malaria hasa kwa Wajawazito na watoto, utafanyika saa chache baada ya kuachiwa rasmi mitaani siku hiyo hiyo ya Jumamosi.
Taarifa toka kwa wasambazaji wa filamu hiyo iliyoshinda tuzo za Golden Hamster katika tamasha la filamu la Northwest Projections, Marekani, kampuni ya Steps Entertainment ni kwamba filamu hiyo itaachia rasmi mitaani siku hiyo na jioni yake itazinduliwa rasmi bure.
"Filamu ya Chumo, ambayo inatarajiwa kuingia mitaani siku ya Jumamosi itazinduliwa rasmi siku hiyo hiyo jioni kwenye viwanja vya Biafra, wakisindikizwa na makundi ya muziki ya Ashimba na Jagwa Music, bila kiingilio chochote," taarifa hiyo ya Steps ilisema.
Filamu hiyo iliyoteuliwa kwenye matamasha ya filamu ya ZIFF, Pan African na Durban International Films Festival, imewashirikisha wasanii kadhaa nyota nchini akiwemo Miss Temeke-2006, Jokate Mwegelo, Yusuph Mlela 'Angelo', Hussein Mkiety na Jafaki Makatu.
Kazi hiyo mpya iliyotararishwa na Jordan Ribery imetayarishwa nchini na Asasi ya MFDI-Tanzania na kufadhiliwa na JHU-CCP kupitia Mfuko wa Rais wa kutokomeza Malaria na Shirika na Misaada la Marekani, USAID.

No comments:

Post a Comment