VISURA waliojitokeza kushiriki shindano la kumsaka mrembo wa mji wa Bagamoyo, 'Vodacom Miss Bagamoyo-2011' wameingia kambini tangu wiki iliyopita tayari kujiandaa na shindano hilo litakalofanyika Mei 28.
Warembo hao 12 wameingia kambini kwenye ukumbi wa New Mzalendo Pub, uliopo jengo la Millenium Tower, jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa onyesho hilo, Awetu Salim, alisema wameamua kuiweka kambi hiyo jijini ili kuwapa urahisi warembo waliojitokeza kushiriki shindano hilo ambalo litafanyikia kwenye ukumbi wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo, TaSUBA, mjini Bagamoyo.
Awetu, alisema karibu asilimia kubwa ya warembo waliojitokeza licha ya kutokea Bagamoyo, lakini shughuli zao nyingi huzifanya Dar es Salaam ambapo wanafanya kazi au kusoma.
"Warembo wetu wameingia kambini kwenye ukumbi wa New Mzalendo Pub, uliopo eneo la Makumbusho, tayari kujiandaa na shindano la Mei 28," alisema Awetu.
Mratibu huyo ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Asilia Decoration, hakuweza kuwataja majina ya visura hao kwa madai, hakuwa na orodha wakati akizungumza na mtandao huu..
"Wapo warembo zaidi ya 12 na tayari wameshanza kunolewa wakipewa mbinu za kuweza kuinuka washindi wa kinyang'anyiro hicho, cha Vodacom Miss Bagamoyo 2011," alisema Awetu.
Awetu alisema katika onyesho lao hilo litapambwa na burudani kamambe toka kwa kundi mahiri la muziki wa taarab la Jahazi Modern 'Wana Naksh Naksh' linaloongozwa na 'Mfalme' Mzee Yusuph.
No comments:
Post a Comment