Monday, May 30, 2011

Bangkok Deal sasa ni Bangkok Dream

SEHEMU ya pili ya filamu ya kutisha ya 'Bangkok Deal' ipo hatua ya mwisho kabla ya kuachiwa
mitaani ikibadilishwa jina na kuitwa 'Bangkok Dream'.
Mkurugenzi wa kampuni ya Huba Film Production, Husseni Ramadhani 'Swagger One' alisema sababu ya kuipa filamu hiyo jina jipya ni kujitofautisha na watayarishaji wengine waliozoea kuendeleza jina la filamu hata katika matoleo zaidi ya mawili.
Swagger, aliyewahi kutamba kwenye muziki na filamu kabla ya kugeukia utayarishaji, alisema
ameona kurejea jina la 'Bangkok Deal' hata katika sehemu hiyo ya pili ni 'ukale' ambao wengine
wanapaswa kufuata mkondo wake.
"Bangkok Dream ni muendelezo wa Bangkok Deal, ila nimeipa jina jipya kuonyesha mfano kwa wengine kuacha kuendekeza 'ukale' wa kutoa filamu kwa jina moja katika sehemu hata nne, hali inayochosha watazamaji wetu." alisema.
Aliongeza filamu hiyo iliyokuwa ikipigwa picha zake eneo la Kigamboni, nje kidogo ya jijini la Dar es Salaam, imekamilika na sasa inafanyiwa uhariri kabla ya kuingizwa sokoni.
Swagger aliyetamba na kundi la Crime Buster, lenye wasanii kadhaa akiwemo Blandina Chagula 'Johari', Renatus Pamba 'Mr Simple' ambaye kwa sasa ni Diwani wa Sinza na Saleh Komba 'Mourin', alisema kazi hiyo mpya ni 'funika bovu' kwa jinsi washiriki walivyoonyesha kiwango, kuliko hata toleo la awali.
"Ninachoomba, wadau wa filamu waisubiri iingie sokoni wapime maelezo yangu, ila ni kazi yenye kiwango cha hali ya juu pengine kuliko 'Bangkok Deal' ambayo ipo kwenye mchakato wa kushirikishwa kwenye Tamasha la Kimataifa la filamu za Zanzibar, ZIFF," alisema.

No comments:

Post a Comment