MWIMBAJI nyota wa muziki wa dansi nchini, Mwinjuma Muumin 'Kocha wa Dunia',
amemuonya mwanamuziki mpya wa Extra Bongo, Ramadhani Masanja 'Banzastone'
akimwambia kama anataka kujiletea mabadiliko kimuziki lazima aachane na masuala ya Ulevi.
Pia, Muumin, alisema kitendo cha Banza kujiunga Extra Bongo kinafanana na alivyowahi kufanya yeye alipojiunga na Ally Choki na kuunda bendi ya Double Extra, ambapo Banza aliifananisha hatua hiyo sawa na kutengeneza kitanda kwa kuunganisha stuli na meza.
Akizungumza na Mtandao huu, Muumin alisema Extra Bongo inaweza kunufaika zaidi na ujio wa Banza endapo mkali huyo ataachana na ulevi na mambo mengine yaliyoshusha kimuziki.
"Kila mdau wa muziki wa dansi ukimuuliza ategemee nini juu ya kuungana kwa Choki na Banza pale Extra Bongo, kwanza atatarajia kusikia makubwa kutoka kwa wanamuziki hao, lakini akitafakari jinsi Banza anavyosumbuka na ulevi, bila shaka atakata tamaa," alisema.
Alifafanua, katika mazingira ya kawaida Banza ni mwanamuziki mkali na nyota lakini siyo siri kuwa ukali wake unaathiriwa na ulevi unaomsababishia ajisahau hivyo kupotea umakini.
Banza alitangaza kujiunga na Extra Bongo wiki chache zilizopita na tayari ameshaizawadia wimbo mpya bendi hiyo unaojulikana kama 'Falsafa' ambao wapenzi wa muziki walipata fursa ya kuusikia 'live' jukwaani wamesifu maneno yaliyotumika na kuonyesha kuwa bado wamo.
Muumin ambaye kwa sasa anaitumikia bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', alisema hataki kuwa mtabiri wa maisha ya watu katika fani, ila anaamini endapo Banza hataacha ulevi ndoto yake ya kuisaidia Extra Bongo itabaki kuwa kitendawili kisichoteguka.
No comments:
Post a Comment