Tuesday, May 17, 2011

Wagombea Villa Squad 'kikaangoni' Jumamosi

WAGOMBEA 14 waliojitokeza kuwania nafasi ya uongozi ndani ya klabu ya Villa Squad wanatarajiwa kufanyiwa usaili wao kesho kabla ya kuanza mbioni za kujinadi kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Juni 12.
Awali uchaguzi huo ulitangazwa ungefanyika Mei 22, lakini kwa mujibu wa makubaliano baina ya Kamati za Uchaguzi za Villa na TFF, uchaguzi huo sasa utafanyika katika tarehe hiyo mpya.
Katibu wa Kamati ya Uchaguzi wa Villa, Frank Mchaki, aliuambia Mtandao huu kuwa, jumla ya wagombea 14 wamejitokeza kuwania nafasi za uongozi katika klabu hiyo ambao kesho watasailiwa kupitisha majina ya watakaochuana kwenye uchaguzi mkuu mwezi ujao.
Alisema kwenye nafasi ya Uenyekiti yupo mgombea mmoja tu, ambaye ni Abdalla Majura Bulembo, huku kwenye nafasiu ya Umakamu Mwenyekiti kuna wagombea wawili wanaowania nafasi hiyo na waliosalia ni wanaozitaka nafasi saba za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
"Usaili wa wagombea wetu utafanyika Mei 21 ambapo watakaokidhi vigezo na sifa watapitishwa kabla ya kusubiri kama kuna mapingamizi yatakayowekwa, kisha wagombea kuanza kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Juni 12," alisema Mchaki.
Villa itafanya uchaguzi huo wiki moja kabla ya kuanza rasmi kwa zoezi la usajili wa wachezaji kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo timu hiyo ni miongoni mwa klabu mpya nne zilizopanda daraja toak Ligi Daraja la Kwanza.
Timu nyingine zilizopanda daraja na Villa ni JKT Oljoro ya Arusha, Coastal Union ya Tanga na Moro United ya Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment