Monday, May 30, 2011

Roman Mng'ande: Mpuliza tarumbeta anayezeekea Msondo Ngoma






MASHABIKI wa Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' walimbatiza jina la 'Romario', wakifananisha utundu na umahiri wake wa jukwaani sawa na aliokuwa nao nyota wa zamani wa Brazil, Romario aliyekuwa mkali wa kufumania nyavu uwanjani.
Hata hivyo, hawakukosea kumpa jina hilo kutokana na ukweli kwamba, kabla ya kutumbukia kwenye muziki akikojifunza kupuliza tarumbeta kwa Father Kanuti, mjini Morogoro, Romario ambaye majina yake kamili ni Roman Mng'ande,  alikuwa mahiri katika soka.
Mng'ande, aliyeitumikia Msondo karibu miaka 30 sasa, alisema enzi akisoma na hata alipoingia kwenye muziki alikuwa mshambuliaji wa kati, akifananishwa na nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Sunday Manara 'Computer'.
"Kabla ya kuingia kwenye muziki, nilikuwa namba 9 hatari nikizichezea timu za Kilakala Stars na timu ya mkoa wa Morogoro katika Taifa Cup, miaka ya 1970," alisema.
"Hata nilipokuja Dar kujiunga Urafiki Jazz mwaka 1980 na nilipotua Juwata niliendelea kucheza nikiwa na timu ya Mwanga All Stars hadi nilipostaafu 1987." aliongeza.
Mng'ande aliyeanza fani za sanaa na michezo tangu akiwa shule ya msingi, alisema alipenda muziki kutokana na kuvutiwa na marehemu Mbaraka Mwinshehe na kurithi kipaji toka kwa wajomba na mama yake.
Alisema, mama yake mzazi ambaye ni marehemu kwa sasa alikuwa mahiri kwa uimbaji wa nyimbo asilia, huku wajomba zake wakipiga magitaa ya kienyeji (galaton) katika shoo za klabu za pombe.
Alisema alichukuliwa na Father Kanuti mwaka 1973, kuendeleza kipaji chake cha kupuliza filimbi alichokianza akiitumikia bendi ya shule na alipohitimu alipiga bendi kadhaa za mtaani wa Morogoro kabla ya kufuatwa na Urafiki Jazz mwaka 1980.
Mwaka mmoja baadaye aliihama Urafiki na kujiunga na Tanzania Stars iliyokuwa ikitumbuiza kwenye ukumbi wa Magoti enzi hizo, kisha kutua Msondo Ngoma enzi ikiitwa Juwata Jazz mwaka 1982 na kibao cha kwanza kukishiriki kikiwa ni 'Faulata'.
Tangu wakati huo hadi leo Mng'ande hajahama Msondo. Ameshiriki albamu zote za bendi hiyo tangu mwaka huo, akiwa ni mmoja wa viongozi na pia rapa.
Kuhusu mafanikio, Mng'ande alisema muziki umemfanya ajenge nyumba tatu, zilizopo Keko Mwanga, Kibamba na Chanika, pia anamiliki mashine za kuchomea vyuma, vyerehani na kuitunza familia yake na kuwasomesha watoto wake.
Mkongwe huyo ana watoto wanne aliozaa na mkewe Letcia Francis aliyeoana naye mwaka 1981, ambao ni Jenifer Mng'ande (28), Daktari anayefanya kazi hospitali ya Mahenge, Morogoro na Stella Mng'ande (25) anajishughulisha na biashara.
Wengine ni Chriss (17) anayejiandaa kumaliza kidato cha nne ambaye pia ni dereva na Rich (10) anayesoma darasa la tano Shule ya Msingi Airwing, Ukonga Dar es Salaam.
Mng'ande alisema hatarajii wanae kumrithi kipaji cha muziki kwa vile amewazuia kujihusisha.
Shabiki huyo wa klabu ya Yanga na Arsenal ya Uingereza, anamzimia mpiga solo, Said Mabela 'Dokta' aliyenaye Msondo Ngoma, akidai ni mwanamuziki anayeujua muziki.
"Huyu jamaa achana naye, anaujua muziki, sisi tuliye karibu 'tunainjoi'. Alistahili kupewa tuzo ya heshima na Kili Music Awards-2011."
Mng'ande, aliyezaliwa Februari 7, 1964 mjini Morogoro akiwa ni mtoto wa tatu kati ya wanne wa Mzee Mng'ande, alisema hakuna tukio la furaha kwake kama lile la mwaka 1979 aliposhikana mkono na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Nyerere.
"Tukio hilo lililotokea tulipoenda kuzima Mwenge huko Butiama, litabaki kichwani hadi milele yote kwa vile ni jambo ambalo sikulitarajia," alisema.
Juu ya huzuni, Mng'ande alisema ni kuwapoteza wazazi wake wawili, hasa kushindwa kumzika mama yake mwaka 1990. Baba yake alifariki miaka mitatu baadaye.
"Kushindwa kumzika mama kutokana na kukosekana kwa mawasiliano nikiwa Dar kunaniuma hadi leo, ila naamini yote ilikuwa ni mipango ya Mungu tu," alisema.
Mng'ande, anayependa kula Ugali kwa Samaki, kinywaji chake kikiwa ni soda, alisema kama angekutana na rais angemuomba  aweke sera za kupunguza ushuru na kodi kwa vyombo vya muziki ili kurahisisha upatikanaji wake na kusaidia wengi kujiajiri.
"Vyombo vya muziki vipo juu na kuwakwaza wengi kuvimiliki, ila mimi ningekuwa rais ningeinua uchumi na kuinua maisha ya wananchi nikiboresha huduma muhimu kama za Afya, Elimu na Kilimo," alisema.
Kuhusu kuporomoka kwa muziki wa dansi, Mng'ande aliyekitaja kibao cha 'Kilio cha Mtu Mzima' kama moja ya kazi ya kujivunia kwake kwa jinsi alivyoitendea haki, alisema hali hiyo inatokana na bendi nyingi kuendekeza tabia ya kuiga kazi za nje.
"Muziki wetu unaporomoka kwa sababu bendi nyingi zinaiga kazi za wanamuziki wa nje na kuwafanya mashabiki watususe kwa kutoona tofauti," alisema.
Tabia ya baadhi ya wanamuziki wameshafika mbali wakati ndio kwanza wanaanza imechangia muziki wa dansi kupoteza kasi yake ya awali.
"Bongofleva nawasifu kwa mafanikio, ila wana tatizo la kuwa wavivu kujifunza kupiga ala ili kwenda na wakati na kukamilika kuwa wanamuziki.
Alisema mazoea ya kupiga muziki kwa kutumia 'Play Back' hautawafikisha kokote.

No comments:

Post a Comment