Monday, May 30, 2011

Mbwana: Sitamsahau Mfilipino aliyening'oa jino ulingoni



KIPAJI chake cha ngumi kilichoanza kuonekana tangu akiwa kinda akirithi kutoka kwa baba na kaka zake, kilimwezesha Mbwana Matumla 'Golden Boy' kupata ajira bila kutarajia ndani ya Jeshi la Polisi mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Bondia huyo maarufu anayeshikilia taji la Ubingwa wa Mabara wa UBO, uzani wa Superfly, alivutwa Polisi tangu akiwa yupo darasa la tano katika Shule ya Msingi Mgulani.
Alisema alichukuliwa na Polisi ili kuichezea timu yao na ngumi na alipomaliza masomo yake ya msingi alipewa ajira mwaka 1993.
Miaka miwili baadae alipelekwa kwenye shule ya uaskari ili kuwa askari kamili, wakati ambao alikuwa tayari alishaisaidia timu hiyo kutamba katika ngumi, huku mwenyewe akijijengea jina anga za kimataifa.
"Huwezi amini niliajiriwa Polisi kama utani baada ya kuwavutia kwa kipaji changu, nakumbuka nilichukuliwa nikiwa darasa la tano, lakini niliajiriwa mwaka 1993 kabla ya kupelekewa 'depo' mwaka 1995," alisema.
Mbwana, aliyetwaa mataji mbalimbali katika ngumi za ridhaa akiwa na Polisi na timu ya Taifa, alisema hata hivyo alilazimika kuacha ajira jeshini mwaka 1997 baada ya  kushawishiwa kuingia katika ngumi za kulipwa zilizompa mafanikio zaidi kimaisha.
"Niliacha kazi Polisi mwaka 1997 na kutumbukia kwenye ngumi za kulipwa kwa ushawishi wa kocha, Norman Hlabane, wa Afrika ya Kusini, aliyekuwa akimnoa kaka Rashid, ndiye aliyenipa hili jina la 'Golden Boy' kwa kukunwa na ukali wangu," alisema.
Mbwana, alisema alipanda ulingoni kwa mara ya kwanza katika ngumi za ridhaa katika  michuano ya wazi na kumpiga Abdul Mgweno aliyeichezea klabu ya Urafiki.
Aliendelea kutamba akiwapiga wapinzani wake na kuteuliwa kwenye timu ya taifa, ambapo aliisaidia kuiletea sifa Tanzania kwa kutwaa medali kadhaa kwenye michuano mbalimbali kabla ya kuhamishia makali yake kwenye ngumi za kulipwa.
Mbwana alilitaja pambano la kwanza kwa ngumi za kulipwa kwake lilikuwa dhidi ya Mussa Njeu aliyempiga kwa KO, raundi ya kwanza na kuingia moja kwa moja kwenye orodha ya mabondia wa Kanda ya Tano mwaka huo wa 1997.
Taji la kwanza kimataifa kwake ni mkanda wa WBU-International alipomchakaza kwa KO ya raundi ya kwanza bondia wa Hungary, Tamas Szakallas, katika pambano lililofanyika Tanzania, Desemba 19, 1998.
Mataji mengine aliyowahi kutwaa ni  WBA, WBN, PABA, WBU, ICB, IBO na UBO anaoushikilia hadi sasa ambapo aliutwaa mara ya kwanza mwaka 2009 kwa kumpiga Mganda, Festus Omondi, na kutetea hivi karibu mbele ya Mkenya Gabriel Ochieng.
Mbali na mikanda hiyo, Matumla, ambaye ni mnazi mkubwa wa timu ya Simba na klabu ya Manchester United ya Uingereza iliyofungwa 3-1 na Barcelona katika fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa usiku wa kuamkia jana, amewahi kutwaa tuzo mbalimbali ikiwemo ile ya Mwanamichezo Bora inayotolewa na TASWA mwaka 1993 na 1998, Shujaa wa Taifa mwaka 2000 na ile ya Guinness Book.

MFILIPINO
Licha ya  kucheza mapambano mengi ya ngumi, Mbwana alisema pambano dhidi ya Mfilipino, Joel Avala, lililofanyika Machi 30, 2001 jijini Dar es Salaam ndilo gumu na lisilosahaulika kichwani mwake.
Alisema hawezi kulisahau pambano hilo gumu ambalo licha ya kushinda, alipoteza jino lake lililong'oka bila ganzi ulingoni baada ya mpinzani wake huyo kumpiga kichwa mdomoni.
"Siwezi kulisahau pambano dhidi ya Joel Avala kwa jinsi lilivyokuwa gumu na kitendo cha kung'oka jino ulingoni kisha kumchakaza mkali huyo kwa kumshinda katika raundi ya saba... kumbuka alikuwa mzoefu kuliko mimi," alisema.
Alitaja pambano jingine gumu kwake ni dhidi ya Edison Torres wa Venezuela aliyempiga mbele ya mashabiki wake na kuunganisha mataji ya WBA-Afrika na la Latin America.
Mbwana, aliyeoana na Susan Rashid na kuzaa nae watoto watatu, Mariam (17), aliyepo kidato cha tatu Shule ya Sekondari Wailes - Temeke, Leila (8), aliyepo darasa la pili Shule ya Msingi Mgulani na Yusuf (1), alimshukuru kocha Habib Kinyogoli kumfikisha alipo.
"Huyu ndiye aliyekuza kipaji changu, licha ya kwamba pia nimepitia mikononi mwa makocha wengine kama Norman Hlabane, Kinyogoli ana mchango mkubwa kwangu na ngumi za Tanzania," alisema.
Mbwana aliyelitaja tukio la kupata mtoto wa kiume (Yusuf) kuwa ndilo la furaha mwake, alisema kucheza kwake ngumi kumemsaidia mengi kama kujenga nyumba mbili, kumiliki kiwanja Ukonga, jijini Dar es Salaam na kuendesha shughuli za biashara.
"Pia, nimeijua dunia kupitia ngumi, nina marafiki wengi, kifupi ngumi zimenisaidia sana," alisema.
Mbwana anayependa kula ndizi kwa nyama na soda aina ya Fanta, alisema mchezo wa ngumi nchini umedorora sasa kwa kuwepo migogoro na kukosekana kwa  wadhamini, akidai angekutana na Rais hicho ndicho kingekuwa kilio chake kwake.
"Ngumi zimetelekezwa licha ya kuitangaza nchi kwa kutoa mabingwa wa dunia, hivyo ningemuomba Rais asaidie ziwe na wadhamini kama alivyofanya katika soka," alisema.
Na kama yeye Mbwana angekuwa angekuwa Rais wa nchi hii, angeboresha huduma zote za jamii, akihakikisha rasilimali za nchi zinasaidia kuinua uchumi kuwanufaisha wananchi wote, pia kusaidia kuinua michezo ili kusaidia ajira kwa wengi.
Mbwana anayekunwa na Floyd Mayweather Jr. kwa umahiri wake wa kutupa ngumi ulingoni, amepanga kustaafu ngumi miaka mitano ijayo ili awe kocha wa mchezo huo.
"Nimepanga kustaafu miaka mitano ijayo niwe kocha kuinua nyota wapya, tayari nimeshaianza kazi hiyo nikishirikiana na kaka Rashid."
Mbwana Ally Matumla, alizaliwa Aprili 8,1975, Dar es Salaam. Ni mtoto wa tano kati ya watoto 11 wa Mzee Ally Matumla, alisoma Shule ya Msingi Mgulani na kujihusisha katika michezo hasa soka, sarakasi kabla ya kugeukia ngumi hadi leo.

No comments:

Post a Comment