Sunday, April 24, 2011
Kitabu cha Assosa chaingia mtaani
KITABU cha mwanamuziki nguli wa muziki wa dansi, Tshimanga Kalala Assosa, kiitwacho 'Jifunze Lingala' kimeingia mitaani, huku mwenyewe akijiandaa kutoa toleo la pili la kitabu hicho kinachofundisha lugha ya Kilingala na Kiswahili.
Akizungumza na mtandao huu, Assosa, alisema kitabu hicho ambacho mbali na kufunza watu Kilingala, pia kina tafsiri ya nyimbo za wanamuziki maarufu wa Kongo na kiliingia sokoni tangu juzi huku kikigombewa kama njugu.
Assosa, alisema tangu akiingize sokoni kitabu hicho kimeshauza kopi zaidi ya 1000, huku akipokea oda kedekede toka kila pembe ya nchi kwa watu wanaokiulizia.
"Aisee kile kitabu changu nimeshakiingiza sokoni, na huwezi kuamini kimekuwa kikinukuliwa kama njugu tofauti na matarajio yangu, hali inayonifariji mno," alisema Assosa.
Mkongwe huyo aliyewahi kuzipigia bendi za Negro Succes, Orchestre Lipualipua, Fukafuka, Le Kamalee, Marquiz du Zaire, Marquiz Original, Mambo Bado, Legho Stars na sasa Bana Marquiz, alisema hakutaraji kama kingegombewa.
Alisema hakuwa na tumaini la kugombewa kwa kitabu chake kutokana na ukweli ndicho cha kwanza kwake kukitoa tangu aamue kujikita kwenye uandikaji wa vitabu, nje ya shughuli zake za muziki anaoendelea nao hadi sasa.
Aliongeza kuwa, hali hiyo unamfanya afikirie kuongeza idadi ya nakala zake, ili kukidhi mahitaji ya mashabiki wanaokiulizia ambacho ndani yake pia kina picha za wasanii wakongwe wa Kongo pamoja na yeye na familia yake.
"Kama watakuwa wanavihitaji pia wanaweza kwenda pale Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, kuna wakala anaviuza pale, au wanipigie katika 0713-240735, wanaweza kukipata," alisema Assosa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment